Waziri wa ulinzi Nigeria ajiuzulu

Waziri wa Ulinzi wa Nigeria Mohammed Badaru Abubakar amejiondoa madarakani wakati taifa hilo likikumbwa na ongezeko la matukio ya kutatanisha ya utekaji nyara hususan watoto wa shule. 

Hatua hiyo imekuja katika kipindi ambacho serikali inapambana kurejesha utulivu kufuatia mashambulizi na utekaji wa watu kwa wingi ulioshuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Rais Tinubu, Bayo Onanuga, Abubakar mwenye umri wa miaka 63 ameondoka kwenye wadhifa huo mara moja kutokana na sababu za kiafya.

Kujiuzulu kwa waziri huyo kunahusishwa pia na shinikizo linalotokana na hali ngumu ya usalama iliyoikumba Nigeria, huku wananchi na wadau wa usalama wakitoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka na madhubuti kukabiliana na tishio linaloendelea kukua.

Ambapo Serikali ya Rais Tinubu inatarajiwa kutangaza mabadiliko au uteuzi mpya wa waziri wa ulinzi katika siku chache zijazo ili kuimarisha juhudi za kurejesha amani na usalama nchini humo.

Aidha kujiuzulu kwake kunafuatia tangazo la Rais Bola Tinubu la kutangaza hali ya dharura ya usalama wa taifa wiki iliyopita. 

Hata hivyo tangazo hilo lililenga kuimarisha juhudi za kukabiliana na wimbi la utekaji lililoripotiwa mwezi uliopita, ambapo mamia ya watu—ikiwemo idadi kubwa ya watoto wa shule—walitekwa ndani ya kipindi kifupi. 

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii