Putin anatarajiwa kukutana na ujumbe maalum wa Marekani kujadili vita ya Ukraine

Rais wa Russia Vladimir Putin anatarajiwa kukutana na mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff mjini Moscow leo Desemba 2 mwaka huu baada ya Ikulu ya White House kusema ina matumaini makubwa ya kufikia makubaliano ya kumaliza vita vya Ukraine.

‎‎Taarifa ya Mkutano huo wa Witkoff na Rais Putin imetolewa na msemaji wa Urusi Dmitry Peskov

‎‎Mkutano huo utafanyika ikiwa ni baada ya mazungumzo ya siku mbili huko Florida kati ya maafisa wa Ukraine na Marekani wakiwemo Witkoff na Kushner yaliyolenga kuboresha mpango wa amani unaoungwa mkono na Marekani, ambao awali ulionekana kuipendelea Urusi.

‎‎‎Akizungumza baada ya mkutano na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron jijini Paris siku ya Jumatatu, Rais Zelensky alisema vipaumbele vya Kyiv katika mazungumzo ya amani ni kulinda uhuru wa Ukraine na kupata dhamana madhubuti za kiusalama.

‎Zelensky alisema kwamba "suala la mipaka ya eneo ndilo gumu zaidi" katika makubaliano ya amani, huku Urusi ikiendelea kushinikiza Ukraine ikubali kuachia maeneo ya Mashariki, ambayo bado inaidhibiti jambo ambalo Kyiv imekuwa ikisisitiza kwa muda mrefu kwamba kamwe haitakubali.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii