Wafungwa 73 wamemaliza mafunzo ya ufundi stadi

WAFUNGWA 73 kutoka magereza mbalimbali nchini wamehitimu mafunzo ya ufundi stadi katika fani mbalimbali Chuo cha Magereza Ruanda jijini Mbeya hatua inayolenga kuwasaidia kupata ajira au kujiajiri pindi watakapomaliza adhabu zao.

Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa amewataka wahitimu hao kutumia ujuzi walioupata kama nyenzo ya kujipatia kipato  na kuwa raia wema watakaporejea katika jamii.

Pia amewasihi wafungwa hao watakapotoka gerezani kuomba kazi halmashauri mbalimbali hasa kwenye idara zinazohitaji mafundi wa ndani ili waweze kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali, Jeremiah Katungu, kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Kamishna wa Magereza, Ahmed Mwen-dadi amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za serikali kuwezesha wafungwa kupata ujuzi utakaosaidia kujitegemea kimaisha baada ya vifungo vyao.

Naye Mkuu wa chuo hicho , Dickson Katabalo, amesema mafunzo hayo yalianza Julai 2024 yakiwa na wanafunzi 82 katika fani za uashi, uselemala, umeme, ufundi bomba, rangi,uchomeleaji pamoja na ushonaji, hata hivyo ni wanafunzi 73 waliomaliza, wakati wengine walishindwa kuendelea na masomo kutokana an sababu mbalimbali.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii