Walimu wavamia shule, watimua wenzao na kula mlo wao

MAMIA ya walimu wanaogoma katika Kaunti ya Uasin Gishu walivamia shule ya upili ya Uasin Gishu ambapo walitorosha wenzao waliokuwa wakifundisha kabla ya kusherekea mlo wa mchana uliokuwa umeandaliwa walimu wa shule hiyo.

Uamuzi wa kuvamia shule hiyo uliafikiwa baada ya juhudi za kukutana na mkurugenzi wa TSC kaunti hiyo kukosa kuzaa matunda.

Walimu hao wakiongozwa na katibu wa tawi Elijah Maiyo pamoja na mwenyekiti, Sosthen Bellat walifika shuleni humo kutaka kujua ni kwa nini wenzao walikuwa wakifundisha wakati mgomo ulikuwa ukiendelea.

Walimu ambao walikuwa wakisimamia mtihani shuleni humo walichana mbuga, huku mwalimu mkuu akidaiwa kujificha msalani.

Wakati wa sarakasi hiyo wanafunzi walishangilia hatua ya walimu waliogoma kuvamia shule yao.

Kinaya ni kwamba wanafunzi ndio walikuwa wakionyesha waandamanaji mahali walimu wao walikuwa wamejificha.

Baadhi ya walimu walionekana wakitorokea katika shamba la mahindi shuleni humo.

Baada ya walimu wa shule hiyo kutoroka, wanachama wa KUPPET waliokuwa wamevalia shati za rangi ya manjamo walipekua shule hiyo kutoka darasa moja hadi jingine kabla ya kufika kwenye chumba cha maakuli ambapo walisherekea mlo wa chamcha uliokuwa umeandaliwa walimu wa shule hiyo.

Waliamrisha wapishi wa shule hiyo kuwapa nyama, huku wakidinda kula sukumu bila nyama.

Ilibidi wapishi kutii na kuwapa nyama ambayo ilikuwa imefichwa jikoni.

“Ninafanya maandamano ya kupigania hawa watu ilihali wao wako hapa wanafurahia minofu, sili ugali kwa sukuma hebu leta hiyo nyama,” aliamuru mmoja wa walimu wa kike ambaye alisimamia shughuli ya kusherekea mlo shuleni humo.

Juhudi za walinzi wa shule hiyo kufunga lango kuu hazikufua dafu, kwani walimu hao walifungua lango hilo kwa lazima baada ya kupanda ua na kuingia ndani ya shule hiyo kufungulia wenzao walioshindwa kupanda ua.

Bw Maiyo alisema walimu wataendelea na mgomo, akidokeza kwamba tawi lake halijapokea agizo la mahakama kusitisha mgomo.

“Sisi tunaendelea na mgomo leo, kesho, kesho kutwa, mtondo na kuendelea hadi tuambiwe na viongozi wetu wa kitaifa mgomo umesitishwa,” alisema Bw Maiyo.

Ajabu ni kwamba, licha ya kuwepo kwa agizo la mahakama kusitisha mgomo huo idadi kubwa ya walimu ilijitokeza mjini Eldoret ikilinganishwa na siku za hapo awali.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii