Mkuu wa shirika la kimataifa waandishi habari wasiokuwa na mipaka - RSF Christophe Deloire amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 53. Deloire aliugua ugonjwa wa saratani.
Katika salamu zake za rambirambi kupitia mtandao wa kijamii wa X, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema fani ya uandishi ilikuwa moyoni mwa Deloire. Kiongozi huyo wa Ufaransa ameongeza kuwa Deloire alipigania bila kuchoka uhuru wa habari na mijadala ya kidemokrasia. Nayo kamati ya kulinda maslahi ya waandishi wa habari iliyo na makao makuu yake mjini New York, CPJ imeandika kwenye mtandao wa X kuwa, "imehuzunishwa mno" na kifo cha Deloire.