Hospitali ya Taifa ya afya ya Akili Mirembe Yazidiwa na Wagonjwa wa Akili

Hospitali ya Taifa ya afya ya Akili Mirembe imetumia Sh70 milioni ndani ya mwaka mmoja kuhudumia wagonjwa 34 wa afya ya akili katika matibabu na malezi yao baada ya kutelekezwa na familia zao.

Wagonjwa hao ni wale waliofikishwa hospitalini hapo na Jeshi la polisi, wasamaria wema na familia zao kwa ajili ya matibabu na baada ya kuwafikisha waliwatelekeza bila kuwafuatilia maendeleo yao.

Akizungumza nasi leo Jumapili Novemba 19, 2023 Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa hospitali hiyo, Christian Alais amesema wagonjwa hao wamekuwa wakisababisha hospitali hiyo kuelemewa na gharama za kuwahudumia.

Alais amesema hospitali hiyo hutumia gharama kubwa ya kuwahudumia wagonjwa hao hasa kwa upande wa chakula kwani kila mmoja hutumia chakula cha Sh6,000 kwa siku ambacho kinagharamikiwa na hospitali.

Mbali na hilo wagonjwa hao wanalala na kuishi hospitalini hapo kwani hata baada ya kupona hawana pa kwenda na wengi wao hawakumbuki walipotoka na hata wale wanaokumbuka hawawezi kurudi makwao na hivyo kubakia hospitalini hapo.

“Tuna wagonjwa 34 ambao wamepona lakini familia zao zimewatelekeza hapa hospitalini na kati yao wanaume wako 18 na wanawake wapo 16 ambao wanaishi na kula hapa hospitalini kwa kuwa hawana mahali pa kwenda,” amesema Alais

Amesema wagonjwa hao ni wale waliokaa muda mrefu bila kufuatwa na familia zao ambapo kuna wengine wamekaa kwa miaka kati ya mitano hadi kumi

Amesema pamoja na hospitali kuwa na utaratibu wa kuchukua namba za simu za ndugu wa wagonjwa lakini baadhi yao hutoa namba ambazo siyo sahihi na hata wale walitoa namba sahihi wakipigiwa huwa wanabadilisha namba hivyo inakuwa vigumu kuwapata tena.

“Na wengine wakisikia ni hospitali ya Mirembe alipoacha mgonjwa ndiyo wanaompigia anasema umekosea namba ili tu usiendelee kumsumbua kuhusu ndugu yake aliyemwacha hospitalini,” amesema Alais

Mkuu huyo wa kitengo amesema hivi sasa Hospitali hiyo inafanya mpango wa kuwatangaza wagonjwa hao ili familia zao ziwaone na kuwachukua ili kuipunguzia hospitali gharama za kuwahudumia.

Daktari wa magonjwa ya akili kutoka Mirembe, Dk Enock Changarawe amesema ili kuiepuesha jamii kutelekeza wagonjwa waliopona ni lazima elimu ya kuishi na watu hao itolewe ili kuondoa hofu iliyopo.

Amesema watu wengi wana hofu kutokana na historia ya mgonjwa hivyo hata wakiambiwa amepona bado wanakuwa na wasiwasi wa kuendelea kuishi naye kwenye jamii.

Mwanasaikolojia Gloria Kasilo, ambaye ni  Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Afya ya Wanawake Tanzania amesema sababu za watu waliopona ugonjwa wa akili  kukataliwa kwenye jamii zipo nyingi ikiwemo jamii kutokuwa na imani nao kuwa wamepona kabisa hivyo wana hofu kuwa wanaweza kuwadhuru muda wowote.

 “Nashauri tujitahidi kufanya machaguo sahihi kwenye maisha yetu ili kuondokana na msongo wa mawazo, sonona, wasiwasi na mashaka, pia kutojiingiza kwenye tabia zisizofaa zinazoweza pelekea kupata magonjwa ya akili kwa sababu mtindo mzuri wa maisha hupunguza magonjwa ya akili,” amesema Gloria

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii