HEKARI 101 NA MAGUNIA 482 YA BANGI YATEKETEZWA ARUSHA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya (DCEA) imefanikiwa  kukamata gunia 482 za bangi iliyokuwa tayari kusafirishwa kwenye masoko na  imeteketeza jumla ya hekari 101 za mashamba ya bangi yanayokadiriwa kuwa na bangi mbichi gunia 550 katika eneo la Kisimiri Juu kata ya Uwalu, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.


Ukamataji huo umefanyika Mei 31,2023 kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya operesheni nchi nzima ili kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa nchini.

Akizungumza operesheni hiyo maalumu iliyofanyika mkoani Arusha Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo amesema, Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama itaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo hayo ili kuhakikisha bangi inatokomea kabisa na hatimaye wakulima na wananchi kwa ujumla wanaoishi katika eneo ya Kisimiri juu na chini wanaachana na kilimo cha bangi na kujikita katika mazao mengine ya biashara badala ya bangi.

Kamishna Lyimo amesema kuwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) katika kuhakikisha agizo la Mheshimiwa Rais linatekelezwa, ameelekeza kufanyika kwa utafiti kujua ni mazao gani mbadala yanaweza kulimwa katika maeneo hayo ambayo yamekithiri kwa kilimo cha dawa za kulevya, ili wananchi wa maeneo husika waweze kupewa mbinu mbadala za kulima mazao mbalimbali ya chakula na biashara badala ya kuendelea na kilimo cha bangi. 


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii