Kifo mikononi mwa Polisi: IGP apeleka timu Chato

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Camillus Wambura, ametuma timu ya Maafisa kutoka Polisi Makao Makuu Dodoma kwenda Kata ya Mganza, Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita kufuatilia tukio la kuchomwa moto kwa Kituo cha Polisi cha Kata hiyo lilitokea Machi 30, 2023.


Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara Kata ya Mganza, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema haiwezekani kutatua kosa la jinai kwa kufanya kosa la jinai na kwamba tukio la kuchoma kituo cha Polisi ni kosa na waliohusika wanatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kujichulia sheria mkononi.

IGP Wambura ameagiza timu hiyo inayoongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Ramadhani Kingai ambaye kufanya pia upelelezi wa tukio la kufariki kwa Enos Misalaba akiwa mikononi mwa polisi kwa kushirikiana na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, David Misime kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi.

Akiongea katika mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Chato, Dkt. Medadi Kalemani alimpongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa hatua hiyo na kusema Jeshi la Polisi pia linatakiwa kujitathmini kwa yaliyotokea na wananchi wajitathmini kwa hatua waliyoichukua ili kujirekebisha na kuanza ukurasa mpya.

Tukio la kituo cha Polisi Mganza kuvunjwa kisha kuchomwa moto na wananchi lilitokea wakati umati wa watu ulipoandamana kupinga kifo cha mtuhumiwa aliyekuwa ameshikiliwa kwa tuhuma za wizi wa betri ya gari.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii