KUFIKIA DESEMBA 2023 WAUGUZI 3000 KUPATA MAFUNZO YA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA NCHINI.

Serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja na wadau wameendelea kutoa mafunzo juu ya magonjwa yasiyoambukiza ambapo hadi kufikia Desemba, 2023 mafunzo hayo yanategemea kuwafikia watoa huduma za Afya Msingi wapatao 3000 kutoka Mikoa yote 26.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji-Hospitali ya Rufaa ya Kanda-Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji wakati akifunga mafunzo ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza yaliyokuwa yakitolewa kwa wauguzi wa mikoa mitano Jijini Mbeya.

“Mafunzo haya ni awamu ya Sita yanatolewa kwa wauguzi 460 kutoka katika vituo vya Afya vya mikoa mitano ambayo ni Mbeya, Katavi, Iringa, Rukwa na Njombe ambapo wamejengewa uwezo katika kuzuia, kudhibiti na kutoa huduma za magonjwa yasiyoambukiza nchini.” Amesema Dkt. Mbwanji

Serikali ipo katika utekelezaji wa Mpango Mkakati Jumuishi wa Tatu wa kuzuia na kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza, Afya ya akili na Ajali mwaka 2021/2025 ambapo unahusisha kuhakikisha watoa huduma wanapewa mafunzo ili waweze kutoa huduma bora za magonjwa yasiyoambukizwa kote nchini katika ngazi zote za utoaji wa huduma za Afya.

“Mpango mkakati huu wa Tatu unalenga kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za Afya ili kuboresha kiwango cha huduma za kinga, tiba na huduma utengamao za magonjwa hayo kuanzia ngazi ya jamii hadi Taifa.” Amesema Dkt. Mbwanji

Aidha, Dkt. Mbwanji amesema moja kati ya mikakati iliyopo ni kuimarisha huduma za msingi kwa kuvijengea uwezo vituo vya Afya 600 kwa kuwapa mafunzo watoa huduma za Afya juu ya utoaji wa huduma za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa upande wake Meneja Mpango-Magonjwa Yasiyoambukiza Dkt. Rachel Nungu amesema mafunzo haya yataendelea katika Mikoa iliyobakia ikiwemo Mkoa wa Ruvuma, Mtwara, Morogoro, Tanga, Manyara, Shinyanga na Tabora.


“Mafunzo haya yatawafikia jumla ya watoa huduma 710 katika vituo vya Afya 172 vya Mikoa hiyo iliyosalia.” Amesema Dkt. Nungu

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii