Polisi waua majambazi waliokuwa na mabomu

Jeshi la Polisi mkoani Kagera limewaua kwa kuwapiga risasi watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, na kufanikiwa kupata bunduki moja aina ya AK47 ikiwa na magazine moja yenye risasi 25 na mabomu mawili ya kutupwa kwa mkono,katika barabara itokayo Kumnazi kuelekea Rulenge wilayani Ngara.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi mkoani Kagera William Mwampaghale amesema kuwa Januari 21 mwaka huu walipata taarifa fiche kuwa kuna watu wanasafirisha silaha kwa pikipiki na kuweka mitego katika barabara zote zinazotoka na kuingia Ngara mjini, na kwamba ilipofika saa 3:35 usiku, katika barabara hiyo walionekana watu watatu wakiwa wamepakizana katika pikipiki moja, na waliposimamisha walikaidi kusimama.

Kamanda Mwampaghale amesema kuwa polisi walifyatua risasi hewani na kuendelea kuwasihi wasimame lakini hawakutii amri hiyo, ndipo askari walifyatua risasi wakilenga kupiga tairi la pikipiki, lakini kwa bahati mbaya risasi hizo zikawapiga abiria wawili waliokuwa wamebebwa katika pikipiki hiyo, wakadondoka chini na kupoteza maisha wakati wakiwahishwa hospitali. 

Kamanda huyo amesema kuwa mtu mmoja aliyekuwa akiendesha pikipiki hiyo alifanikiwa kukimbia na kuwatoroka.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo kuuawa kwa watu hao na kupatikana kwa silaha hizo kumetokana na oparesheni inayoendelea katika mkoa wa Kagera ambayo inaishirikisha mikoa jirani ya Shinyanga, Kigoma na Geita.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii