Wanasheria Chad kususia kazi

Wanasheria nchini Chad wameapa kususia kazi leo, wakati itakapoanza kesi ya halaiki inayohusisha watu zaidi ya 400 waliokamatwa katika maandamano yenye ghasia ya kuipinga serikali.

Kulingana na takwimu rasmi, watu 50, kumi miongoni mwao wakiwa maafisa wa usalama waliuawa katika maandamano hayo yaliyofanyika katika mji mkuu, N’Djamena tarehe 20 Oktoba.

Hata hivyo upinzani unasema idadi ya waliopoteza maisha ni kubwa zaidi, na kuwa raia wasio na silaha waliuawa.

Kesi ya watuhumiwa hao inatarajiwa kusikilizwa hadi Desemba 4, katika gereza lenye ulinzi mkali la Koro Toro lililo katikati mwa jangwa, umbali wa kilomita 600 kaskazini mwa mji mkuu.

Mafaili ya mwendeshamashitaka wa serikali yanaonyesha kuwa watu 621 walikamatwa katika maandamano, na uchunguzi unafanyika kujua waliko watu 220 ambao hawahusishwi kwenye kesi inayoanza leo Jumanne, miongoni mwao wakiwemo 83 wasiotimiza umri wa utu uzima.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii