Uingereza yatetea uamuzi wa kujiondoa Umoja wa Ulaya licha ya matatizo ya kiuchumi

Waziri wa fedha wa Uingereza Jeremy Hunt ametetea hatua ya nchi yake ya kujiondoa Umoja wa Ulaya licha ya kuongezeka kwa lawama juu ya athari za kiuchumi zilizosababishwa na hatua hiyo.

Waziri huyo wa fedha pia amekanusha madai kwamba analenga kuleta uhusiano wa karibu kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Waziri Hunt aliyepiga kura ya kutaka Uingereza ibakie kwenye jumuiya hiyo anatuhumiwa kuwa chanzo cha ripoti ya mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba serikali ya Uingereza inakodolea macho uhusiano na Umoja wa Ulaya kama ule uliopo kati ya Uswisi na jumuiya hiyo. Uswisi haimo katika Umoja wa Ulaya lakini ina mkataba wa biashara huru na jumuiya hiyo.

Hata hivyo waziri huyo wa fedha wa Uingereza Jeremy Hunt amesisitiza kuwa yeye siye chanzo cha taarifa zilizonukuliwa kwenye vyombo vya habari kwamba Uingereza inataka uhusiano wa karibu na Umoja wa Ulaya.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii