Rais wa Ukraine azishukuru Marekani na Umoja wa Ulaya kwa msaada

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy leo ameishukuru Marekani kwa msaada ziada wa dola bilioni 40 ulioidhinishwa na Bunge mjini Washington jana ili kuisaidia nchi hiyo kiuchumi na kijeshi kutokana na uvamizi wa Urusi. Kupitia hotuba kwa taifa aliyoitoa usiku wa kuamkia leo, Zelenskyy amesema msaada huo ambao unajumuisha fedha za kununua silaha, huduma za kiutu na kupiga jeki shughuli za uzalishaji unadhihirisha uongozi imara wa Washington katika kulinda uhuru. Zelenskyy pia ameushukuru Umoja wa Ulaya kwa kuiunga mkono nchi yake akisema mchango wa kanda hiyo utazuia kuzuka kwa vita vyengine ambavyo Urusi inaweza kuvianzisha iwapo itapata ushindi nchini Ukraine. Katika hatua nyingine, Marekani imetangaza kuwa inatuma silaha nzito zenye thamani ya dola milioni 100 nchini Ukraine ambazo ni tofauti na zile zitakazonunuliwa kupitia kitita cha dola bilioni 40 zilizoidhinishwa na Bunge hapo jana.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii